Wednesday 19 March 2014

UHURU WA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA.


Uhuru wa Vyombo vya Habari Nchini Tanzania bado ni Utata mtupu kutokana na Urasimu wa Sera na Ukiritimba uliopo katika Utoaji na upashanaji wa Habari.

Ijapokuwa Tanzania imeridhia na Inatambua Mikataba mbalimbali ya Kimataifa juu ya Haki na Uhuru wa Vyombo vya Habari lakini bado inasuasua katika utoaji wa Uhuru huo kwa kile kinachodaiwa kuwa wahusika wanalinda Masilahi yao Binafsi au ya wale walio Viongozi au Wakubwa wao.

Katika kuthibitisha kuwa Tanzania Imeridhia Mikataba ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari inaungana na Jamii ya Kimataifa kila Mwaka Kuadhimisha siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari May’3 ikiwa ni Pamoja na Viongozi wa Serikali,Vyama,NGO’s,Mabalozi na Taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa kuungana na Vyombo vya Habari katika Maadhimisho hayo.

Katika Maadhimisho hayo Vyombo vya Habari huungana Pamoja na Kubainisha Changamoto wanazokutana nazo katika Utendaji wao wa Kila siku mbele ya Jamii na Taifa kwa ujumla.

Waandishi wa Habari Nchini Tanzania pamoja na Kuwa kiungo muhimu sana kati ya Serikali na Wananchi bado hawathaminiwi wala kupewa nafasi stahiki katika kuwawezesha kuandika na kuripotisha Habari kwa wakati na kwa muda wa Muafaka.

Matukio Mbali mbali ya Unyanyasaji na Udhalilishaji wa waandishi wa Habari wakiwa Kazini yameripotiwa na Vyombo vya Habari ikiwa ni Pamoja na Tukio ambalo halitasahaulika katika Tasnia ya Habari la Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Television ya Channel Ten Mkoani Iringa NdgDaudi Mwangozi 2012.

Tukio lingine litakalokumbukwa na Vyombo vya Habari Nchini Tanzania ni la Kutekwa,Kupigwa na Kujeruhiwa Vibaya kwa Mwenyekiti wa Jukwaa laWahariri wa Vyombo vya Habari Bw Absalom Kibanda March 5’2013 hali iliyompelekea Kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na baadaye kupelekwa Afrika ya kusini kwa Matibabu zaidi.


Haya  ni Miongoni mwa Matukio yaliyojitokeza na katika tasinia ya Habari nchini Tanzania ikiwa Sanjari na Matukio Mengine yaliyojiri yakiwa na Lengo la kuziba Midomo Vyombo vya Habari Nchini Tanzania pasipo kujali wala kukumbuka kuwa Kuwanyima Vyombo vya Habari Uhuru ni Kuwanyima Haki ya Kikatiba Watanzania kwa Mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Said Kubenea (Picha kwa Hisani ya Mwanahalisi Publishers).
Matukio mengine ya kutisha dhidi ya Waandishi wa Habari Nchini Tanzania ni lile la Kumwagiwa Tindikali Mwandishi wa Gazeti la Mwanahalisi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mwana Halisi Bw Said Kubenea na Baadaye Gazeti hilo kufungiwa na Serikali kwa kile kilichodaiwa kuwa limeandika Habari za Kichochezi.


Pamoja na Gazeti la Mwana Halisi kufungiwa hali hiyo pia imekumba Gazeti la Mwananchi lililofungiwa siku 14 na Mtanzania lilifungiwa Siku 90.

Hatua ya Serikali Kufungia na Kunyima Uhuru Vyombo vya Habari ni Changamoto kubwa sana kwa Vyombo vya Habari Nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kutotolewa kwa Taarifa juu ya Hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya wale wote waliotuhumiwa kuhusika Kumuuwa Mwangosi,Kuwateka,Kuwapiga na Kuwajeruhi Waandishi wa Habari.

Watanzania hasa wale wa Vijiji wanategemea Vyombo vya Habari hasa Radio katika Upataji wa Habari Mbali mbali za Kitaifa na hata za Kimataifa kwani Radio ni Chombo cha Gharama ya Chini kidogo ukilinganisha na Tv au Gazeti,hivyo kunyima vyombo vya Habari Uhuru na hata kuwanyima nafasi ya kuripoti Matukio muhimu kwa Jamii ni Kuwaumiza Wananchi.

Bunge la Maalum la Katiba lilipoanza Vikao vyake Februari 18’2014 Mjini Dodoma,Waandishi wa Habari walinyimwa fursa ya kuripoti Taarifa za Bunge hilo ingawa Watanzania wa Mijini na Vijijini walikuwa na hamu ya kufahamu nini kinafanyika Bungeni na nini hatma yao kuelekea kupata Katiba Mpya.

Pamoja na Kutambua kuwa ni Haki ya watanzania kuhabarishwa Kamati ya Bunge Maalum imepitisha Kanuni ya kanuni ya kuwazuia waandishi wa habari kuingia katika vikao vya kamati za chombo hicho, hatua ambayo ni kinyume na Katiba inayotoa uhuru wa wananchi kupata habari.

Pamoja na  Waandishi wa Habari kukutana na Vikwazo,Manyanyaso,Udhalilishaji na Hata baadhi Kuumizwa bado hawajakata Tamaa wala Kurudi nyuma kuwasemea Watanzania walio Wanyonge wasio na Sauti na Wale wa Tabaka la chini.

Udhibiti wa Habari pia bado ni Changamoto inayojitokeza kwa Baadhi ya Vyombo vya Habari hasa katika Eneo la Utamaduni,Mila,Lugha,Jinsia,Watoto na Jamii za Pembezoni(Wafugaji,Wawindaji na Waokota Matunda) kwani kumekuwepo na hali ya Kuandika na Kuripoti Habari za Mijini zaidi kuliko Vijijini ingawa Matukio mengi yanatokea maeneo hayo.

Habari za Maeneo ya Vijijini zimekuwa zikiandikwa na kuripotiwa tu pale inapotokea Ziara ya Viongozi wa ngazi ya Juu Serikalini,Mf;Rais,Makamu wa Rais,Waziri Mkuu au Waziri anapotembelea eneo hilo.

Upatikanaji wa Habari kwa Vyombo vya Habari bado nayo ni Changamoto kutokana na Urasimu uliopo katika baadhi ya Vyanzo vya Habari,Mf;Taasisi za Serikali,NGO’s,Mashirika ya Umma,etc hali inayodumaza Uwazi na Uwajibikaji Nchini Tanzania.

Pamoja na Vyombo vya Habari Nchini Tanzania Kukosa Uhuru kamili wanakabaliwa pia na Ukosefu wa Raslimali na Ujuzi katika Utendaji  wao wa kila siku jambo linalopelekea kutoandika au kuripoti taarifa kwa wakati huku tasnia ya Habari ikivamiwa na wasiokuwa na Wito wa Taaluma hiyo ya Habari(Makanjanja).

Umiliki wa Vyombo vya Habari Nchini Tanzania umeendelea kuimarika na kukua siku baada ya siku kwa Serikali kutoa Leseni na Fursa ya Uanzishwa wa Vyombo vya Habari TV,Radio na Magazeti kwa Watu Binafsi,Mashirika ya Kiserikali na Binafsi,Vyama vya siasa,Taasisi za Dini na Mashirika ya Kimataifa ijapokuwa Vyombo hivyo vinakandamizwa katika kupewa nafasi ya Kuhabarisha Umma wa Watanzania.
Uanzishwaji wa Vyombo vya Habari pia imeleta Changamoto ya Vyombo hivyo kutumika kupigana Vijembe na kuleta Uhasama ndani ya Jamii kwa wale wanaotumia vyombo hivyo kwa maslahi yao Binafsi na shughuli wanazofanya,Mf;Mvutano uliotokea baina ya Rostam Aziz na Reginal mengi.

Ukosefu wa Mishahara ya Kutosha na Marupurupu mengine ni tatizo kubwa katika Tasnia ya Habari Nchini Tanzania hasa kwa Vyombo vya Habari vya binafsi hali inayopelekea baadhi ya Waandishi wa Habari kujiingiza katika Vitendo Haramu ikiwa ni pamoja na kupokea Rushwa tofauti na Nchi Jirani ya Kenya ambayo Waandishi wa Habari wanalipwa Vizuri.
 



 

No comments:

Post a Comment